Michael Shuma,Upupu:
Ni
wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini
umzima na unaendelea nyema na maandalizi ya sikukuu za Christmas na
Mwaka Mpya.
Mimi
namshukuru Mungu kwa kila jambo ambalo amekuwa akinitendea katika kila
siku ya maisha yangu na nimuombe tu anijaalie niwe miongoni mwa wale
watakaouona mwaka 2015 wakiwa wazima.
Mpenzi msomaji wangu, kilio cha wengi walio kwenye uhusiano ni
kusalitiwa na wapenzi wao waliotokea kuwaamini sana. Wapo ambao si tu
kwamba wanahisi bali wanawafumania kila kukicha waume/wake zao licha ya
imani waliyokuwa nayo kuwa hawawezi kusalitiwa.
Imefika wakati baadhi yetu hatutaki hata kufuatilia nyendo za wenza
wetu tukijua kwamba kufanya hivyo ni kujitafutia presha za bure. Labda
mimi naweza kuwa na uelewa tofauti katika hili la kufuatilia nyendo za
wapenzi wetu. Ninachojua mimi ni kwamba, ili uwe na amani moyoni mwako
juu ya mwenza wako lazima uthibitishe kama kweli anakupenda na ametulia.
Utafanya hivyo kwa kufuatilia nyendo zake bila yeye kujua na katika
kufuatilia kwako ndipo utajua kama kweli umempata mwenza sahihi ama laa.
Wapo ambao husimamia kwenye ule msemo kwamba, ukimchunguza sana bata
humli! Jamani ule ni msemo tu, tunajua kila mmoja ana mapungufu yake ila
ni vyema ukayajua ya wako ili ujue namna sahihi ya kuishi naye.
Nalazimika kusema haya kwa kuwa, kasi ya wapenzi kusalitiana imekuwa
ikishika kasi kila siku kiasi cha baadhi kuhisi bila kusaliti hawasikii
raha. Yaani wanapatilizwa kila kitu na wenza wao lakini bado wanatoka
nje.
Unakuta mwanaume ana mke mzuri anayejua mapenzi na kila kitu lakini
bado mwanaume huyo haridhiki. Pia wapo wanawake ambao wamebahatika
kuwapata wanaume ‘handsome’, wanaojua mapenzi na kujali pia lakini bado
tamaa za usaliti wanakuwa nazo. Ukiuliza kipi kigeni wanachofuata huko
nje, jibu hakuna.
Watu wa sampuli hii ni vyema kuwabaini kuliko kubaki na ile imani
kwamba, anakupenda na hawezi kukusaliti. Una ushahidi gani kama kweli
anakupenda na hakusaliti huko anakopita?
Hivi leo ukiambiwa utaje
sababu inayokufanya uamini kuwa mwenza wako hachepuki utatoa sababu
gani? Hakika huwezi kuwa nayo, sanasana utaishia kusema unamuamini kwa
kuwa hujawahi kumfumania wala kuona dalili za kuzungukwa.
Kizuri ni kwamba, ukifuatilia sana utagundua wengi wetu hutuna imani
ya asilimia 100 ya kutosalitiwa. Wengi wetu licha ya wenza wetu
kuonyesha wametulia, bado hatuwaamini kupitiliza. Hii yote ni kwa sababu
akiamua kukusaliti anaweza kufanya hivyo na wewe usijue lolote.
Nilishawahi kufanya uchunguzi huko nyuma kwa kuzungumza na baadhi ya
watu kuhusu hili suala la kusalitiwa. Wengi walikiri kujua kwamba
wanasalitiwa lakini wenyewe wanadai ni mambo ambayo wakiyafuatilia
hawawezi kudumu kwenye ndoa zao.
Ni kweli niliobahatika kuongea nao kwenye hili ni wachache sana
lakini maelezo yao yamenifanya niwe na uhakika wa hiki ninachokiandika
leo.
Kipi kifanyike?
Kutokana na maelezo yangu hapo juu utakubaliana
na mimi kwamba hakuna anayeweza kusimama mbele za watu na kuthibitisha
kuwa hasalitiwi. Kikubwa ni wewe na mimi kuwaamini wapenzi wetu.
Lakini pia hakuna ubaya kama utafuatilia na kujua kama kweli uliye naye
ametulia na hachepuki. Usibaki kuamini kibubusa kwamba husalitiwi,
wakati mwingine fuatilia nyendo zake bila yeye kujua.
Najua kweli ukifanya hivyo unaweza kugundua madudu mengi kwa huyo
uliyenaye na ukajikuta unachanganyikiwa lakini ni bora utakuwa umejua
yaliyojificha ili uchague mwenyewe kusuka au kunyoa.
Heri ujue
kisha kama huwezi kumuacha, uzungumze naye, abadilike kuliko umuache
aendelee kufanya ufuska wake gizani kisha wewe ubaki na imani kwamba
ametulia na hawezi kukusaliti.
Lakini kama moyo wako unagoma kumfuatilia mpenzi wako na moyo wenyewe
unakuhakikishia kwamba mwenza wako katulia, basi baki na imani yako
hiyo.Lakini kwa ulimwengu wa sasa kama utakuwa umejihakikishia kwa
asilimia 100 kwamba una mpenzi ambaye hajawahi kukusaliti na wala
hafikirii, jiweke kwenye kundi la watu waliobahatika na Mungu awabariki
sana.