Saturday 13 December 2014

Leave a Comment

SHITUKA WEWE! UTAISHI KWENYE NYUMBA YA KUPANGA MPAKA LINI?

Maisha siku zote ni kuwa na malengo, namaanisha malengo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Kwamba unaishi huku ukijua mwaka huu utafanya jambo flani na mwaka kesho utafanya jambo flani.
Cha ajabu sasa wapo watu ambao hawana malengo yoyote, wanaishi ili mradi siku zinakwenda.
Hili ni tatizo na ukijaribu kufuatilia utagundua wote wanaoishi bila malengo wana maisha magumu na wameridhika nayo. Yaani hawajui kesho yao itakuwaje na wala hawataki kujishughulisha kujua.
Ilimradi leo Mungu kawajaalia wamekula, wanaona hawana sababu ya kufikiria kesho watakula nini. Hii ni shida!
Katika hilo leo nataka kuwazungumzia wale wenzangu na mimi ambao tunaishi kwenye nyumba za kupanga. Ukifuatilia sana utagundua ni wachache sana ambao hawakuwahi kuishi kwenye nyumba za kupanga, hasa maeneo ya mjini.
Naweza kusema hiyo ni hatua ya tulio wengi katika kuelekea kwenye kumiliki nyumba zetu. Hapa namaanisha kwamba, wengi wetu tumeanza maisha tukiwa tumepanga chumba kimoja, baadaye tukachukua chumba na sebule na hatimaye tukapanga nyumba nzima kadiri vipato vyetu vilivyokuwa vinaongezeka na familia kuwa kubwa.
Lakini katika maisha ya sasa utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakuwa unawaza kupanga tu na wala hufikirii siku moja kuwa na nyumba yako na ikiwezekana uwapangishie wengine.  Nasema haya nikimaanisha kwamba, wapo watu huko mtaani ambao wao wamechukulia maisha ya kupanga kama sehemu ya maisha yao. Yaani hawawazi kumiliki nyumba, walipokuwa mabachela, walipanga, walipooa bado waliendelea kupanga na huenda sasa wana familia lakini bado wanapanga na hawana mikakati ya kuwa na ‘mijengo’ yao.
Walio katika mazingira hayo wajue wanajiandaa kuzeeka wakiwa kwenye nyumba za kupanga, jambo ambalo ni baya sana. Ifike wakati ukae na kujiuliza kwamba, wale ambao walianza kwenye nyumba za kupanga lakini sasa wanaishi kwenye nyumba zao huku nao wakiwa na wapangaji wao wana kipato gani kikubwa kukushinda wewe?
Marafiki na wafanyakazi wenzako ambao huenda mnapokea mshahara sawa wamejenga, wewe pesa zako zinaishia wapi? Au unaona kujenga siyo ishu? Kwamba hata usipojenga ilimradi una sehemu ya kuishi na mambo yanakwenda sawa, basi poa?
Mimi nadhani unakosea, kumbuka ipo siku utakuwa huna pesa ya kupanga, nguvu zimeisha na una familia ambayo inahitaji uihifadhi. Kama utakuwa hujajijengea kakibanda kako katika wakati huu ambao una kazi na Mungu anakujaalia unapata vijisenti, huoni ipo siku utajuta?
Mimi nakushauri kwamba, kama unafanya kazi au una vipato vingine na hujajenga, wala huna malengo hayo, ni vyema ukaanza sasa. Weka mikakati ya kuhakikisha unakuwa na nyumba yako. Jinyime kama wanavyofanya wenzako. Kumbuka ni wachache sana ambao walijenga baada ya kupata pesa nyingi, wengi walidhamiria siku moja kuachana na mambo ya kupanga, wakawekeza kidogokidogo, mara wakanunua viwanja, wakaanza msingi na hatimaye kusimamisha nyumba. Sasa wanaishi kwao na wengine ni baba wenye nyumba/mama wenye nyumba, kinachokushinda wewe ni kipi?
Tena mbaya zaidi baadhi ya waliojenga nyumba zao unaweza kukuta wanapata pesa ndogo kuliko hizo unazopata wewe, huoni umefika wakati wa wewe kufikiria kuwa na nyumba yako? Tafakari kisha ni vyema ukachukua hatua.

0 comments: