Saturday 6 December 2014

Leave a Comment

RAHA YA MAFANIKIO YAKO USAIDIE NA WENGINE WAFANIKIWE!

Mpenzi msomaji wangu, unapojaaliwa kuwa na mafanikio jambo la kwanza unatakiwa kumshukuru sana Mungu pamoja na wale ambao kwa namna moja ama nyingine wamekufanya ufike hapo ulipo.Huwezi kufanikiwa kwa ujanja wako, mafanikio yako yote nyuma yake kuna mkono wa Mungu. Yeye ndiye anayeweza kuziona jitihada ulizonazo na akaona akutimizie ndoto zako. Ukiacha yeye, wapo watu mmojammoja au kwa vikundi na taasisi ambao wamechangia wewe kuwa na mafanikio uliyo nayo. Hawa ni watu wa kuwaheshimu sana. Kamwe usiwasahau, endelea kuwa nao karibu kwani umuhimu wao kwako ni mkubwa sana.
Aidha, unapofanikiwa na wewe unatakiwa kuwa chachu ya mafanikio kwa wengine. Unatakiwa kuwashika mkono ndugu, marafiki na watu wengine wanaokuzunguka ili watoke kwenye hali duni walizonazo. Ukifanya hivyo utazidi kupaa kimafanikio na hata siku moja huwezi kuporomoka.
Ipo mifano mengi ya watu ambao wamefanikiwa lakini wanakosa furaha kuwaona watu wanaowazunguka bado wanaogelea kwenye dimbwi la umasikini.Hawa utawaona wakiwa mstari wa mbele kuwasaidia wengine kimawazo na hata kifedha ili nao wainuke na waweze kutimza ndoto zao.
Iko wazi kwamba bosi wangu, Eric Shigongo ni miongoni mwa watu wenye mafanikio makubwa. Kama uliwahi kusoma popote kuhusu historia ya maisha yake, utaona ni jinsi gani amepambana kufika hapo alipo.
Kinachotia moyo zaidi ni kwamba, licha ya mafanikio aliyonayo, hajaridhika, bado anaendelea kupambana na kuzidi kujiwekea malengo makubwa zaidi.
Lakini licha ya mafanikio yake, bosi wangu huyu ambaye pia ni mwalimu wa ujasirimali amekuwa akitumia muda wake mwingi kutoa elimu kwa watu mbalimbali juu ya namna wanavyoweza kutoka kwenye umaskini na kuingia kwenye utajiri.
Amekuwa akifanya hivyo kupitia vitabu vyake, kwenye makongamano na semina mbalimbali akieleza njia ambazo yeye amepita mpaka akafikia hapo alipo sasa. Ukiacha elimu anayotoa, pia amekuwa akiwasaidia wengi kifedha ili waweze kutimiza ndoto zao. Hiki ndicho ambacho watu waliofanikiwa wanatakiwa kukifanya.
Huwezi kuendelea kuwa kwenye mafanikio kama utakuwa mchoyo wa kuwafanya na wengine wafanikiwe. Utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakuwa unataka ufanikiwe wewe tu na wengine waendelee kuwa mafukara.
Hivi utakuwa ni mtu wa aina gani kama una pesa nyingi lakini umekuwa mgumu kuwasaidia wale ambao wanahitaji msaada kutoka kwako? Faida ya wewe kufanikiwa ni ipi sasa kwa jamii yako?Mimi nadhani kuna kila sababu ya wale ambao wamefanikiwa kuona wana jukumu la kuwasaidia na wengine kufanikiwa.
Kama si kwa kuwapa mitaji basi hata kwa kuwapa mawazo ambayo yanaweza kubadili fikira zao.
 Usijenge mazingira ya kwamba wewe tu ndiye unayestahili kuishi vizuri, wasaidie na wengine waishi maisha ya furaha. Kumbuka faida ya kufanya hivyo ni kubwa sana.
Kwanza Mungu atakuongezea mafanikio yako na utashangaa kila unalolipanga linatimia. Pia, jamii inayokuzunguka itakupenda na itakuona ni mtu unayejali wengine.
Kwa maana hiyo unapofanikiwa usijitenge na jamii inayokuzunguka. Saidia pale inapopidi, washike mkono wengine waweze kusimama. Kumbuka siku wakiwa wamefanikiwa, ile tu kusema ‘flani kanisaidia mimi kufika hapa’, Mungu anakuzidishia baraka na unashangaa mambo yanazidi kukunyookea.

0 comments: