Wednesday, 17 December 2014

Leave a Comment

UNATAKA KUPATA UTAJIRI WA HARAKA? SOMA HAPA

HAISHANGAZI kama ukilala maskini ukaamka tajiri. Swali ni je, utaufanyia nini utajiri huo? Amini usiamini inawezekana. Kumbuka, sijasema itakuwa rahisi, nilichokisema ni kwamba inawezekana. Hapa nakuletea dondoo za namna ya kupata utajiri haraka kwa lugha ya mtaani fastafasta.
WEKEZA
Anza kuwekeza ukiwa mdogo yaani kiumri na kidogo ulichonacho. Inawezekana ukaanza hata ukiwa shule ya msingi au hata kama ni shule ya awali sawa tu. Kinachohitajika ni mazingira rafiki ya ujasiriamali. Nakuhakikishia kuwa fedha zako zitaongezeka kila kukicha ukizingatia mambo mengine nitakayoeleza baadaye.
Ni kama mayai yanayotagwa na ndege ambayo baadaye huatamiwa na kuzalisha ndege wengine.
Angalizo; kama unafuatilia makala haya wakati umri umekutupa mkono na hukuweza kuanzia shule za awali lakini una watoto, unaweza kuwatumia kwa kuwatengenezea mazingira ninayoyaeleza. Uwe mwalimu wa ujasiriamali kwa watoto wako au hata wajukuu zako.
Hata kama umri umekwenda lakini Mungu kakujalia kibarua, jaribu kuwekeza asilimia 50% ya mshahara wako katika kujitoa kwa kiwango cha hali ya juu kabisa kutokana na mfumuko wa bei katika soko huru na ugumu wa maisha.
Una uwezekano wa asilimia 50 kwa 50 kutengeneza utajiri au kuanguka ndani ya siku 90.

OA AU OLEWA NA MTU TAJIRI
Najua hapa utakuwa na maswali mengi kwamba nisipooa au kuolewa na mtu tajiri basi nitakufa masikini. Inawezekana pia japo ni kwa asilimia ndogo! Twende mbele zaidi, yaani usemi huu unamaanisha uwe na mwenza wa maisha mwenye maono. Yawezekana msiwe na utajiri kwa maana ya fedha lakini mkawa matajiri wa mawazo ya kijasiriamali. Pale mmoja anapofikia ukomo wa mawazo na kuhisi kushindwa, basi mwenza wake awe nguzo ya kushauri na siyo kukatisha tamaa kabisa kuwa sasa tumeshindwa! Hapana, muote ndoto tofauti lakini mshirikiane kuzitafsiri ili kufikia mafanikio.

SHINDA BINGO
Hii haimaanisha kuwa utajiri unatokana na michezo ya kubahatisha pekee lakini pia inawezekana ila ni kwa asilimia ndogo. Kumbuka wapo waliozaliwa na bahati zao wakashinda michezo ya kubahatisha wakawa matajiri, mifano ipo. Falsafa ni kwamba ujijengee tabia ya kujaribu kufanya vitu. Hapa narudi kipengele cha kwanza yaani kuwekeza hata katika kitu ambacho huna hakika kama utafanikiwa.
Wajasiriamali wanasema ‘ku-take risk’. Haitashangaza kuona unafanikiwa ghafla na wasiamini katika kujaribu wakaishia kusema unatumia ndumba.
WAZAZI MATAJIRI
Kama umezaliwa katika familia tajiri, ukawa na maono katika ujasiriamali, wewe upo nusu ya safari ya mafanikio. Unachotakiwa kufanya ni kuwa mtiifu kwa kupita kwenye nyayo za baba na mama ukiwashawishi kwa kuwa mwangalifu katika matumizi ya kile wanachokupatia. Usitumie kwa kutupatupa ili wakitangulia mbele ya haki ubaki kuwa vizuri tofauti na inavyotokea kwa baadhi ya familia. Jenga nao ushirikiano wa hali ya juu na wakati mwingine wape mawazo hata kama watayaona ni ya kitoto lakini utakuwa umejijengea mazingira ya wao kukuona sehemu ya utajiri wao.

NENDA SHULE UPATE UJUZI
Elimu ni mtaji mkubwa kuliko hata fedha. Jitahidi kusoma katika mazingira yoyote bila kujali wingi wa miaka utakayopoteza darasani. Jaribu kupata weledi na ujuzi wa kila namna halafu chagua kimoja ambacho kitakupa fedha nyingi.
Itaendelea wiki ijayo.

0 comments: