Monday 15 December 2014

Leave a Comment

ACHA KULA UJANA, PAMBANA SASA KUSAKA MAFANIKIO!

Niwakumbushe tu kwamba, licha ya sarakasi zote tunazofanya kwenye maisha yetu ya kila siku, ni vyema tukamtanguliza Mungu na kufanya yale ambayo ametuamrisha na kuachana na aliyotukataza. Kwa kufanya hivyo atatubariki na mambo yetu yatatunyookea.
Baada ya kusema hayo, sasa nirudi kwenye mada yangu ya wiki hii. Mpenzi msomaji wangu, ukweli ni kwamba kila mmoja wetu angependa kuwa na maisha mazuri au kifupi kwamba awe na fedha nyingi, kwa maana ya tajiri.
Hii ndiyo sababu mara kadhaa umepata kusikia juu ya watu wanaosaka utajiri kwa njia mbalimbali, zikiwemo haramu na ushirikina.
Katika dhana ya kusaka mafanikio, kama lengo la kila mmoja ni kutafuta kazi za ndoto zake au kuanzisha kampuni mpya, vijana wengi wanaweza kuweka malengo yao na kufanikiwa haraka kama wataamua.
Wapo watu wengi waliofanikiwa kushika kiasi cha shilingi milioni moja ya kwanza maishani mwao wakiwa na umri chini ya miaka 30 na hapo ndipo mawazo ya wao kuwa mamilionea yalipochipukia. Hakuna uchawi wowote waliowahi kuufanya ili kuwafikisha walipo sasa.
Nafahamu kwamba inawezekana kuwa na maisha mazuri mapema katika maisha yako kama kweli umedhamiria na ukaamua kupigana.
Kama mfanyakazi kijana, watu wengi watauona umri wako kama tatizo kubwa la kufikia malengo yako. Lakini ukweli ni kwamba ujana wako unaweza kuwa na msaada mkubwa sana kwako.
Wengi niliowahi kufanya nao kazi na biashara walikuwa ni watu wazima, wakati mwingine walikuwa wakubwa kuliko mimi.
Hawa wote walikuwa wanataka kufikia malengo yao lakini baadhi hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kufika huko wanakofikiri.
Walihitaji kutokea kwa mtu mwenye dhamira na nia anayeifahamu vyema biashara wanayotaka kuifanya.
Hata hivyo, bado kuna hasara pia kwa kuwa kijana na mtu asiye na uzoefu katika kazi au ujasiriamali, lakini unapoamua kukubali umri wako na kuazimia kupigana kuelekea mafanikio, lazima uwaambie watu unaotaka kushirikiana nao kuwa wewe kweli ni kijana, lakini hilo halimaanishi kwamba huelewi unachokifanya, unajua na umedhamiria kuwa bora katika uwanja unaoingia.
Unapobaini kipaji chako, ni lazima ujitoe kukitumia ili kiweze kukupa maisha unayotamani. Na katika hili, usiwe mtu wa kuwa peke yako kimawazo, jaribu kushirikiana na unaowaamini katika mawazo yako, kwamba unafikiri kuhusu kufanya hivi na vile, wasikilize wanavyokushauri, lakini mwisho wa siku ni lazima uamue kwa faida yako mwenyewe.
Nina uhakika yupo mtu sahihi, bila kujali umri wake ambaye mara nyingi hutokea kuwa mkubwa kuliko wewe, atakayekubaliana na mawazo yako na kuamua kuungana na wewe katika kuyafanyia kazi.
Niseme tu kwamba, wewe kijana huu ndiyo muda wako wa kupambana na kusaka mafanikio kwa nguvu zote.
Waliocheza enzi za ujana wao, sasa wanakiona cha mtemakuni. Acha kula ujana, tengeneza maisha yako ya baadaye sasa!

0 comments: