Showing posts with label mahusiano. Show all posts
Showing posts with label mahusiano. Show all posts

Saturday 13 December 2014

ISHU SI KUOA, ILA UNAMUOA NANI KWA VIGEZO GANI?-2

Na Michael Shuma:
Kwa moyo mkunjufu nikukaribishe mpenzi msomaji wa safu hii ya Love and Story, tunapata kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo maisha ya uhusiano.
Kwa wale tulioianza mada ya ishu siyo kuoa, ila unamuoa nani kwa vigezo gani wiki iliyopita, hakika wataungana nami kwamba ili uishi usije kujutia ndoa yako, yakupasa kuchagua mke au mume sahihi.
Tunaimalizia mada hii ambapo hakika itakuwa ni funzo kwa pande zote mbili, mwanaume na mwanamke.
Kwenye ndoa kuna wakati wa maradhi. Yawezekana ukaumwa wewe au akaumwa hata ndugu yako, je mkeo atakuwa tayari kukuhudumia. Mbaya zaidi ugonjwa wenyewe unaweza kuwa wa kutia kinyaa, atakuwa tayari kukuhudumia au kuwahudumia ndugu zako?
Lazima ujue kwamba anaweza kustahimili katika hali kama hiyo au maneno yale ya kwamba; “mtaishi kwa shida na raha” yeye atayageuza na kuwa tayari kwa maisha ya raha tu, ya shida hayawezi.
Asiwe mtu wa kwenda na wakati asiyetaka hata kucha zake zisiingie maji kwa kuosha vyombo. Hajui kufua nguo.
Asije kuwa yule wa kufanyiwa kila kitu na dada wa kazi. Yeye ni mtu wa kuelekeza kila kitu halafu dada afanye, suala la kupika kwake ni kizungumkuti.
Mwanamke wa aina hiyo hafai kuwa mama wa watoto. Unafikiri atawafundisha nini wanaye? Ujinga tu!
Mke ndiyo msiri wako, ndiye ambaye anaweza kukushauri kitu pale fikra zako zinapokutana na vikwazo. Siku hazifanani, leo waweza kuwa vizuri lakini kuna siku unaweza kuwa na mawazo, hapo ndipo anapopaswa kutumia nafasi yake kama mke kukurudisha katika hali ya kawaida.
Marafiki zangu, tukubaliane tu kwamba mkeo ndiye mtu pekee ambaye unatumia muda mwingi zaidi kuwa naye karibu. Utakuwa kazini ambako mnashirikiana na wafanyakazi wenzako kwa saa kadhaa  lakini utarudi nyumbani ambako utatumia muda mwingi zaidi kuwa na mwenzako.
Hivyo basi asipokuwa mtu sahihi kwako ni dhahiri kwamba atakuangusha. Lazima uwe na mke ambaye anawaza maendeleo awe anajua anapaswa kufanya nini pindi tatizo linapotokea, asijekuwa mtu wa kulikimbia tatizo.
Awe mvumilivu katika kipindi ambacho uchumi utayumba ndani ya nyumba. Ajue kwamba wewe ndiye mumewe katika hali yoyote. Asije akawa mwepesi kukusaliti kwa sababu tu ameona mpo katika kipindi kibaya kiuchumi.
Badala ya kukusaliti au kukukimbia, anapaswa kufikiri zaidi juu ya mbinu mbalimbali za kujinasua katika tatizo linalowakabili. Badala ya kukaa kusubiri kuletewa kila kitu basi pengine na yeye aweze kubuni miradi midogomidogo ambayo inaweza kupunguza makali ya ugumu wa maisha.
Elimu hii si ya wanaume pekee, wanawake nao wanapaswa kuitumia ili kuweza kujua sifa za mwanaume ambaye anafaa kuwa mumewe. Usikurupuke kuolewa na mtu ambaye huna imani naye au kwa kigezo kwamba pengine ana uwezo wa kifedha.
Lazima ujue ni mtu ambaye anaweza kustahimili shida na raha. Atakuwa bega kwa bega pale wewe utakapohitaji msaada wake? Vinginevyo usikubali, mpe muda wa kutosha kumjua tabia yake. Kama kuna kitu unaona hakipo sawa na kinaweza kurekebishika basi jaribu kumshauri na ukiona hawezi basi ni vyema ukaachana naye usije kujuta baadaye.
Kila mmoja wenu anapaswa kuoa au kuolewa na mtu ambaye anakidhi na hali ya aina yoyote. Ndoa si lelemama, haina majaribio, mkikubaliana basi hakuna kugeuka nyuma!
+

ISHU SI KUOA, ILA UNAMUOA NANI KWA VIGEZO GANI?-1

Na Michael Shuma,Upupu:
VITABU mbalimbali vya dini vinatufundisha umuhimu wa ndoa. Najua wengi tutakuwa tunafahamu juu ya huu mstari ambao upo kwenye Biblia; “Naye mwanamke atamuacha baba na mama yake, ataambatana na mumewe na kuwa mwili mmoja.”
Marafiki zangu, mstari huo una maana kubwa sana. Ndoa ina mapana yake katika maisha ya mwanadamu. Ndoa si kufuliana nguo wala si kufanya tendo la ndoa peke yake. Ndoa inahusisha vitu vingi ambavyo wanandoa inabidi washirikiane.
Ili ndoa idumu, wanandoa lazima wawe wanaendana kwa kila jambo. Waelewane, wavumiliane, wawe na upendo wa dhati na siyo wa kuigiza.Marafiki zangu, kwenye dunia hii iliyojawa na changamoto nyingi, wanandoa wanapaswa kufarijiana, kutiana moyo ili kuweza kuvuka vizingiti na mitihani mbalimbali ya maisha.
Ndoa ni ya watu wawili. Si kitu cha kufuata mkumbo, eti kisa fulani kaoa basi na wewe uoe. Ukioa kwa kufuata fasheni, itakula kwako kama wasemavyo vijana wa kisasa.
Mke ambaye utaishi naye ndani kwa kipindi chote cha maisha yenu lazima awe na sifa za kuwa mke. Ajue kwamba ndoa ina shida na raha, anapoona utamu wake atambue pia kuna uchungu wake, kuna siku shida inaweza kutokea.
Ajue namna ya kukabiliana nayo, hawezi kulikimbia tatizo wakati tayari ameshaingia ndoani.
Wanaume wengi sana wanakosea sana kwenye eneo hili, asilimia kubwa huwa wanaendeshwa na matamanio ya mwili. Anamtamani mwanamke mzuri basi akili yake inaamini kwamba anafaa kuwa mke.
Anasahau kabisa kwamba kuna kitu kinaitwa tabia. Hajiulizi mara mbilimbili kwamba mtarajiwa wake ana tabia njema? Hana muda wa kumtazama mtarajiwa wake kama anaweza kuwa mvumilivu.
Hawazi kabisa kwamba kuna kipindi cha maradhi, anasahau kwamba kuna wakati uchumi unaweza kuyumba ndani ya nyumba, atavumilia?Ili kujua vizuri tabia ya mwenzako lazima utenge muda mzuri wa kumchunguza umpendaye kabla ya kufanya maamuzi. Usikurupuke maana maamuzi ya dakika tano yanaweza kukugharimu maisha yako yote.
Tumia muda mwingi wa kushirikiana na mwenzako ili uweze kumsoma tabia zake. Tabia ya mtu ni kama ngozi, kuibadili ni ngumu sana. Mtu hawezi kuficha tabia yake hata iweje, atadanganya miezi miwili lakini wa tatu atajisahau, utagundua tu.
Utakapoigundua tabia yake ina mapungufu, usikurupuke kumuacha. Muelekeze, mpe muda wa kubadilika na kama ni mtu wa kubadilika, anaweza kubadilika. Ukiona habadiliki katika kipindi fulani basi ni bora ukaachana naye mapema kabla hamjafika mbali ili kuepuka maumivu mazito baadaye.
+

KUNA UBAYA GANI KUFUATILIA NYENDO ZA MPENZI WAKO?


Michael Shuma,Upupu:
Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini umzima na unaendelea nyema na maandalizi ya sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya.Mimi namshukuru Mungu kwa kila jambo ambalo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu na nimuombe tu anijaalie niwe miongoni mwa wale watakaouona mwaka 2015 wakiwa wazima.
Mpenzi msomaji wangu, kilio cha wengi walio kwenye uhusiano ni kusalitiwa na wapenzi wao waliotokea kuwaamini sana. Wapo ambao si tu kwamba wanahisi bali wanawafumania kila kukicha waume/wake zao licha ya imani waliyokuwa nayo kuwa hawawezi kusalitiwa.
Imefika wakati baadhi yetu hatutaki hata kufuatilia nyendo za wenza wetu tukijua kwamba kufanya hivyo ni kujitafutia presha za bure. Labda mimi naweza kuwa na uelewa tofauti katika hili la kufuatilia nyendo za wapenzi wetu. Ninachojua mimi ni kwamba, ili uwe na amani moyoni mwako juu ya mwenza wako lazima uthibitishe kama kweli anakupenda na ametulia.
Utafanya hivyo kwa kufuatilia nyendo zake bila yeye kujua na katika kufuatilia kwako ndipo utajua kama kweli umempata mwenza sahihi ama laa. Wapo ambao husimamia kwenye ule msemo kwamba, ukimchunguza sana bata humli! Jamani ule ni msemo tu, tunajua kila mmoja ana mapungufu yake ila ni vyema ukayajua ya wako ili ujue namna sahihi ya kuishi naye.
Nalazimika kusema haya kwa kuwa, kasi ya wapenzi kusalitiana imekuwa ikishika kasi kila siku kiasi cha baadhi kuhisi bila kusaliti hawasikii raha. Yaani wanapatilizwa kila kitu na wenza wao lakini bado wanatoka nje.
Unakuta mwanaume ana mke mzuri anayejua mapenzi na kila kitu lakini bado mwanaume huyo haridhiki. Pia wapo wanawake ambao wamebahatika kuwapata wanaume ‘handsome’, wanaojua mapenzi na kujali pia lakini bado tamaa za usaliti wanakuwa nazo. Ukiuliza kipi kigeni wanachofuata huko nje, jibu hakuna.
Watu wa sampuli hii ni vyema kuwabaini kuliko kubaki na ile imani kwamba, anakupenda na hawezi kukusaliti. Una ushahidi gani kama kweli anakupenda na hakusaliti huko anakopita?
Hivi leo ukiambiwa utaje sababu inayokufanya uamini kuwa mwenza wako hachepuki utatoa sababu gani? Hakika huwezi kuwa nayo, sanasana utaishia kusema unamuamini kwa kuwa hujawahi kumfumania wala kuona dalili za kuzungukwa.
Kizuri ni kwamba, ukifuatilia sana utagundua wengi wetu hutuna imani ya asilimia 100 ya kutosalitiwa. Wengi wetu licha ya wenza wetu kuonyesha wametulia, bado hatuwaamini kupitiliza. Hii yote ni kwa sababu akiamua kukusaliti anaweza kufanya hivyo na wewe usijue lolote.
Nilishawahi kufanya uchunguzi huko nyuma kwa kuzungumza na baadhi ya watu kuhusu hili suala la kusalitiwa. Wengi walikiri kujua kwamba wanasalitiwa lakini wenyewe wanadai ni mambo ambayo wakiyafuatilia hawawezi kudumu kwenye ndoa zao.
Ni kweli niliobahatika kuongea nao kwenye hili ni wachache sana lakini maelezo yao yamenifanya niwe na uhakika wa hiki ninachokiandika leo.
Kipi kifanyike?
Kutokana na maelezo yangu hapo juu utakubaliana na mimi kwamba hakuna anayeweza kusimama mbele za watu na kuthibitisha kuwa hasalitiwi. Kikubwa ni wewe na mimi kuwaamini wapenzi wetu.
 Lakini pia hakuna ubaya kama utafuatilia na kujua kama kweli uliye naye ametulia na hachepuki. Usibaki kuamini kibubusa kwamba husalitiwi, wakati mwingine fuatilia nyendo zake bila yeye kujua.
Najua kweli ukifanya hivyo unaweza kugundua madudu mengi kwa huyo uliyenaye na ukajikuta unachanganyikiwa lakini ni bora utakuwa umejua yaliyojificha ili uchague mwenyewe kusuka au kunyoa.
Heri ujue kisha kama huwezi kumuacha, uzungumze naye, abadilike kuliko umuache aendelee kufanya ufuska wake gizani kisha wewe ubaki na imani kwamba ametulia na hawezi kukusaliti.
Lakini kama moyo wako unagoma kumfuatilia mpenzi wako na moyo wenyewe unakuhakikishia kwamba mwenza wako katulia, basi baki na imani yako hiyo.Lakini kwa ulimwengu wa sasa kama utakuwa umejihakikishia kwa asilimia 100 kwamba una mpenzi ambaye hajawahi kukusaliti na wala hafikirii, jiweke kwenye kundi la watu waliobahatika na Mungu awabariki sana.
+