Saturday, 13 December 2014

Leave a Comment

ISHU SI KUOA, ILA UNAMUOA NANI KWA VIGEZO GANI?-2

Na Michael Shuma:
Kwa moyo mkunjufu nikukaribishe mpenzi msomaji wa safu hii ya Love and Story, tunapata kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo maisha ya uhusiano.
Kwa wale tulioianza mada ya ishu siyo kuoa, ila unamuoa nani kwa vigezo gani wiki iliyopita, hakika wataungana nami kwamba ili uishi usije kujutia ndoa yako, yakupasa kuchagua mke au mume sahihi.
Tunaimalizia mada hii ambapo hakika itakuwa ni funzo kwa pande zote mbili, mwanaume na mwanamke.
Kwenye ndoa kuna wakati wa maradhi. Yawezekana ukaumwa wewe au akaumwa hata ndugu yako, je mkeo atakuwa tayari kukuhudumia. Mbaya zaidi ugonjwa wenyewe unaweza kuwa wa kutia kinyaa, atakuwa tayari kukuhudumia au kuwahudumia ndugu zako?
Lazima ujue kwamba anaweza kustahimili katika hali kama hiyo au maneno yale ya kwamba; “mtaishi kwa shida na raha” yeye atayageuza na kuwa tayari kwa maisha ya raha tu, ya shida hayawezi.
Asiwe mtu wa kwenda na wakati asiyetaka hata kucha zake zisiingie maji kwa kuosha vyombo. Hajui kufua nguo.
Asije kuwa yule wa kufanyiwa kila kitu na dada wa kazi. Yeye ni mtu wa kuelekeza kila kitu halafu dada afanye, suala la kupika kwake ni kizungumkuti.
Mwanamke wa aina hiyo hafai kuwa mama wa watoto. Unafikiri atawafundisha nini wanaye? Ujinga tu!
Mke ndiyo msiri wako, ndiye ambaye anaweza kukushauri kitu pale fikra zako zinapokutana na vikwazo. Siku hazifanani, leo waweza kuwa vizuri lakini kuna siku unaweza kuwa na mawazo, hapo ndipo anapopaswa kutumia nafasi yake kama mke kukurudisha katika hali ya kawaida.
Marafiki zangu, tukubaliane tu kwamba mkeo ndiye mtu pekee ambaye unatumia muda mwingi zaidi kuwa naye karibu. Utakuwa kazini ambako mnashirikiana na wafanyakazi wenzako kwa saa kadhaa  lakini utarudi nyumbani ambako utatumia muda mwingi zaidi kuwa na mwenzako.
Hivyo basi asipokuwa mtu sahihi kwako ni dhahiri kwamba atakuangusha. Lazima uwe na mke ambaye anawaza maendeleo awe anajua anapaswa kufanya nini pindi tatizo linapotokea, asijekuwa mtu wa kulikimbia tatizo.
Awe mvumilivu katika kipindi ambacho uchumi utayumba ndani ya nyumba. Ajue kwamba wewe ndiye mumewe katika hali yoyote. Asije akawa mwepesi kukusaliti kwa sababu tu ameona mpo katika kipindi kibaya kiuchumi.
Badala ya kukusaliti au kukukimbia, anapaswa kufikiri zaidi juu ya mbinu mbalimbali za kujinasua katika tatizo linalowakabili. Badala ya kukaa kusubiri kuletewa kila kitu basi pengine na yeye aweze kubuni miradi midogomidogo ambayo inaweza kupunguza makali ya ugumu wa maisha.
Elimu hii si ya wanaume pekee, wanawake nao wanapaswa kuitumia ili kuweza kujua sifa za mwanaume ambaye anafaa kuwa mumewe. Usikurupuke kuolewa na mtu ambaye huna imani naye au kwa kigezo kwamba pengine ana uwezo wa kifedha.
Lazima ujue ni mtu ambaye anaweza kustahimili shida na raha. Atakuwa bega kwa bega pale wewe utakapohitaji msaada wake? Vinginevyo usikubali, mpe muda wa kutosha kumjua tabia yake. Kama kuna kitu unaona hakipo sawa na kinaweza kurekebishika basi jaribu kumshauri na ukiona hawezi basi ni vyema ukaachana naye usije kujuta baadaye.
Kila mmoja wenu anapaswa kuoa au kuolewa na mtu ambaye anakidhi na hali ya aina yoyote. Ndoa si lelemama, haina majaribio, mkikubaliana basi hakuna kugeuka nyuma!

0 comments: