Saturday, 13 December 2014

Leave a Comment

ISHU SI KUOA, ILA UNAMUOA NANI KWA VIGEZO GANI?-1

Na Michael Shuma,Upupu:
VITABU mbalimbali vya dini vinatufundisha umuhimu wa ndoa. Najua wengi tutakuwa tunafahamu juu ya huu mstari ambao upo kwenye Biblia; “Naye mwanamke atamuacha baba na mama yake, ataambatana na mumewe na kuwa mwili mmoja.”
Marafiki zangu, mstari huo una maana kubwa sana. Ndoa ina mapana yake katika maisha ya mwanadamu. Ndoa si kufuliana nguo wala si kufanya tendo la ndoa peke yake. Ndoa inahusisha vitu vingi ambavyo wanandoa inabidi washirikiane.
Ili ndoa idumu, wanandoa lazima wawe wanaendana kwa kila jambo. Waelewane, wavumiliane, wawe na upendo wa dhati na siyo wa kuigiza.Marafiki zangu, kwenye dunia hii iliyojawa na changamoto nyingi, wanandoa wanapaswa kufarijiana, kutiana moyo ili kuweza kuvuka vizingiti na mitihani mbalimbali ya maisha.
Ndoa ni ya watu wawili. Si kitu cha kufuata mkumbo, eti kisa fulani kaoa basi na wewe uoe. Ukioa kwa kufuata fasheni, itakula kwako kama wasemavyo vijana wa kisasa.
Mke ambaye utaishi naye ndani kwa kipindi chote cha maisha yenu lazima awe na sifa za kuwa mke. Ajue kwamba ndoa ina shida na raha, anapoona utamu wake atambue pia kuna uchungu wake, kuna siku shida inaweza kutokea.
Ajue namna ya kukabiliana nayo, hawezi kulikimbia tatizo wakati tayari ameshaingia ndoani.
Wanaume wengi sana wanakosea sana kwenye eneo hili, asilimia kubwa huwa wanaendeshwa na matamanio ya mwili. Anamtamani mwanamke mzuri basi akili yake inaamini kwamba anafaa kuwa mke.
Anasahau kabisa kwamba kuna kitu kinaitwa tabia. Hajiulizi mara mbilimbili kwamba mtarajiwa wake ana tabia njema? Hana muda wa kumtazama mtarajiwa wake kama anaweza kuwa mvumilivu.
Hawazi kabisa kwamba kuna kipindi cha maradhi, anasahau kwamba kuna wakati uchumi unaweza kuyumba ndani ya nyumba, atavumilia?Ili kujua vizuri tabia ya mwenzako lazima utenge muda mzuri wa kumchunguza umpendaye kabla ya kufanya maamuzi. Usikurupuke maana maamuzi ya dakika tano yanaweza kukugharimu maisha yako yote.
Tumia muda mwingi wa kushirikiana na mwenzako ili uweze kumsoma tabia zake. Tabia ya mtu ni kama ngozi, kuibadili ni ngumu sana. Mtu hawezi kuficha tabia yake hata iweje, atadanganya miezi miwili lakini wa tatu atajisahau, utagundua tu.
Utakapoigundua tabia yake ina mapungufu, usikurupuke kumuacha. Muelekeze, mpe muda wa kubadilika na kama ni mtu wa kubadilika, anaweza kubadilika. Ukiona habadiliki katika kipindi fulani basi ni bora ukaachana naye mapema kabla hamjafika mbali ili kuepuka maumivu mazito baadaye.

0 comments: