HUU ni ukatili namba moja kwa wanandoa duniani! Bado picha haijatoka
kichwani kwa wakazi wa Manzese jijini Dar kufuatia kifo cha kuchinjwa
cha Josephine Ndengaleo Mushi kinachodaiwa kufanywa na mume wake wa
ndoa, Remy Joseph (35).
Remy Joseph (35) anayetuhumiwa kumuua mke wake, Josephine Ndengaleo Mushi.
Tukio hilo la kutisha kusimuliwa achilia mbali kuona, lilijiri saa 9:
10 alasiri ya Januari 29, mwaka huu ndani ya chumba kimoja kilichopo
ghorofa ya pili ya Hotel Friend’s Corner Ltd iliyopo Manzese Argentina,
Dar.
KAMA KAWAIDA YA GAZETI LA UWAZ! Kama kawaida ya
Gazeti la Uwazi, kufuatilia matukio makubwa ya kutisha, kusikitisha na
hata kufichua maovu. Baada ya habari za mauji hayo kusambaa kama moto wa
kifuu, waandishi wetu walianza kuichimba habari hii kwa kina.
SIKU MOJA KABLA YA TUKIO Kwa mujibu wa mhudumu
mmoja wa hoteli hiyo, Januari 28, mwaka huu, Remy na Josephine walifika
kwenye hoteli hiyo na kuchukua chumba. Walionekana wenye amani, kwani
hakuna sura iliyoonesha kuna tatizo.
“Walikuwa kama wateja wengine. Tena niliwauliza kama wanatoka mkoa,
wakasema ni wakazi wa Dar es Salaam, wao ni mke na mume kwa ndoa,
waliamua kulala hapa ili kuimarisha mapenzi yao, si lazima kila siku
nyumbani,” alisema mhudumu mmoja.
JANUARI 29, SAA 9 ALASIRI, DAMU ZAONEKANA Kwa
mujibu wa baadhi ya wahudumu wa hoteli hiyo, siku ya pili, muda wa saa
tisa alasiri, walishtuka kuona damu nyingi ikitoka ndani ya chumba
walichopanga wawili hao.“Tulishtuka sana. Tukajua kuna kitu kikubwa
kimewapata. Ilibidi tuwagongee mlango ili tujue kilichowapata lakini
mlango haukufunguliwa,” alisema mhudumu mwingine.
Mtuhumiwa Remy Joseph akiwa chini ya ulinzi mkali.
POLISI WAITWA Kwa vile ukimya ulitawala ndani ya
chumba hicho huku damu zikiendelea kutiririka, ilibidi uongozi wa
hoteli hiyo yenye sifa ya ulinzi, uwasiliane na Kituo cha Polisi cha
Ndugumbi ambacho kipo jirani.
Polisi walifika, wakagonga mlango kwa
muda mrefu bila kufunguliwa mpaka baadaye sana ambapo mlango huo
ulifunguliwa na mwanaume akiwa ameshika kisu mkono wake wa kuume.
POLISI WATUMIA MBINU YA KIVITA Ndani ya chumba
kulionekana damu zimetapakaa kila sehemu. Polisi walimsihi mwanaume huyo
kuangusha kisu chini ili waongee lakini jamaa aligoma.
“Polisi walimwamuru mwanaume atupe kisu chini, akakataa. Sura yake
wakati huo ilikosa mwonekano wa ubinadamu. Ndipo askari mmoja alitumia
mbinu ya kivita, alimpiga mkono wake wa kulia kwa kumshutikiza kisu
kikaangukia mbali, akawekwa chini ya ulinzi. Kumbe kile kisu mbali na
kumuua mkewe alikitumia kujaribu kujichinja koo lakini ikashindikana,”
alisema mhudumu huyo.
MWILI WA MAREHEMU WAKUTWA UMEPIGISHWA MAGOTI
Mwanaume akiwa chini ya ulinzi na pingu mikononi, polisi waliingia
chumbani na kukuta damu kila mahali. Cha kusikitisha zaidi, mwili wa
marehemu Josephine ulipigishwa magoti, sehemu ya miguu mpaka magoti
ikiwa sakafuni na kifuani kulalia kitanda. Halafu ulifunikwa shuka.“Kwa
mbali ungeweza kusema kuna binadamu anasali kwa namna ambavyo marehemu
huyo alivyokuwa amepigishwa magoti,” alisema mhudumu huyo.
ALITAKA KUJINYONGA Katika hali iliyoonesha kuwa,
mtuhumiwa baada ya kutenda ukatili huo alitaka kujinyonga, polisi
walikuta waya wa umeme wa tivii ukining’inia kwenye pangaboi lakini
ukiwa umekatika.
Remy Joseph akichukuliwa na Polisi kuchukuliwa hatua za kisheria.
UCHUNGUZI WA POLISI CHUMBANI Polisi walifanya
uchunguzi chumbani na kugundua kuwa, marehemu Josephine alichinjwa
shingoni, akakatwa mbavu mbili, moyo na maini vilikuwa nje
‘vikimwagika’, mwisho alichomwa kisu utosini.
LAINI ZA SIMU ZAKUTWA ZIMEKATWAKATWA Pia kwenye
chumba hicho, polisi walikuta simu mbili, ya marehemu na ya mtuhumiwa
zikiwa zimeharibiwa laini kiasi cha kukosa mawasiliano.
UWAZI LAZUNGUMZA NA MTUHUMIWA Uwazi lilipata
bahati ya kuzungumza na mtuhumiwa huyo kabla ya kupelekwa Kituo cha
Polisi Magomeni, Dar ambapo alisema Josephine alikuwa mke wake na
wameishi kwa muda zaidi ya miaka kumi na kupata watoto wawili. Hata
hivyo, hakuongea zaidi ya hapo.
UONGOZI WA HOTELI WATOA NENO Msimamizi mkuu wa hoteli hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Zuberi Hussein alipohojiwa na Uwazi alisema:
“Tuliwapokea hawa watu kama wateja wengine. Walilipa shilingi elfu kumi
na tano kwa chumba. Hatukujua kama haya yangetokea, wahudumu ndiyo
walibaini baada ya kuona damu ikitiririka mlangoni.”
MWILI WA MAREHEMU WAPELEKWA MUHIMBILI Baadaye,
polisi waliupakiza mwili wa marehemu kwenye gari kuupeleka Hospitali ya
Taifa Muhimbili huku mtuhumiwa akipelekwa Kituo cha Polisi Magomeni
jijini Dar pembeni yake akiwa amelala marehemu mkewe.
WANACHOJUA NDUGU WA MAREHEMU Baada ya hapo,
Uwazi lilifunga safari hadi eneo la Studio, Kinondoni, Dar nyumbani kwa
David Ndeshao Mushi ambaye ni kaka wa marehemu na ndiko sehemu
ulipowekwa msiba.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walidai kwamba, Josephine na mumewe mara kwa mara walikuwa na migogoro ya ndoa.
“Ndoa yao haikutulia, walikuwa wanapatanishwa lakini baada ya muda
mfupi wanaanza tena ugomvi. Mumewe alikuwa akimhisi vibaya mke wake.
Hata hivyo, Desemba mwaka jana, Josephine alienda kuishi kwa kaka yake
kutokana na ugomvi,”alisema mmoja wa wanandugu wa karibu.
Kaka mtu huyo alipohojiwa alisema: “Marehemu alirudi kwangu lakini
tulikuwa hatujaongea naye kuhusu ugomvi wao. Nilisafiri mkoani
nikamuacha, niliporudi, Jumatano alienda kazini lakini hakurudi.
Tulipopiga simu yake akawa hapatikani. Mumewe naye akawa hapatikani hadi
taarifa ilipotufikia kwamba kauawa hotelini.
“Tunatarajia kusafirisha mwili kwenda Moshi, Jumapili (juzi). Mazishi
yatakuwa Jumatatu (jana). Marehemu ameacha watoto wawili ambao walikuwa
wakiishi Tabata, Dar.”
MTUHUMIWA, MAREHEMU Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa
alikuwa mfanyakazi wa Baa ya Break Point iliyopo jijini Dar. Marehemu
alikuwa mfanyakazi katika Kampuni ya TAC iliyopo Upanga, Dar.
Mmoja wa marafiki zake wa karibu alisema Jumatano mchana, mumewe
alimfuata kazini na wakawa na mazungumzo, alimtaka waondoke lakini
marehemu alikataa.Alimbembeleza sana mwishowe wakakubaliana na kuondoka
lakini wakashangaa kusikia alimuua hotelini.