Monday 29 December 2014

Leave a Comment

SASA UNAWEZA KUWEKA PESA BENKI KUPITIA ATM


Mteja wa Benki ya NBC, Francis Xavier (kushoto), akiweka fedha katika mashine ya ATM ya benki hiyo wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Katikati ni Meneja wa ATM na Kadi wa NBC, Wambura John (katikati) na Meneja Huduma za Jamii wa benki hiyo, Irene Peter.
Benki ya NBC, imezindua huduma mpya ya kuweka fedha kwenye mashine za ATM jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni moja ya mikakati ya benki hiyo katika juhudi zake za kuboresha huduma za kifedha nchini.

Kuanzishwa kwa huduma hiyo kunathibitisha malengo ya benki hiyo ya kutoa huduma sahihi na ya wakati kwa wateja wake nchi nzima na huduma hiyo ya kuweka fedha kwenye mashine za ATM, itakuwa ikipatikana saa 24 kila siku.

“Uanzishwaji wa huduma hii ya kuweka fedha kwenye mashine za ATM, itawahakikishia wateja wetu kupata huduma sahihi na ya uhakika wakati wowote, uwekaji wa fedha katika mashine hizi ni wa haraka, rahisi na inaokoa muda wa kupanga foleni ndani ya benki,” alisema Mkuu wa Njia Mbadala za Kibenki wa NBC, Raymond Mutagahywa.

Aliongeza kwamba huduma hiyo kwa mtumiaji yeyote ni ya kirafiki na rahisi.

Alifafanua kuwa mteja anatakiwa kufanya mambo machache baada ya kuingiza kadi yake ya ATM na kuchagua sehemu ya kuweka fedha na mashine ya ATM itafunguka ili mteja aweke fedha zake.

Benki hii ya NBC imeanza huduma hiyo kwenye matawi yake ya jijini Dar es Salaam, Karikaoo, Kinondoni, Mlimani City na tawi la makao makuu ambayo mteja anaweza kuweka mpaka Sh. milioni 1.5 kwenye mashine za ATM.

Uzinduzi huo wa kuweka fedha kwenye mashine za ATM, ulifanyika katika tawi la benki hiyo la Mlimani City na kushuhudiwa na wateja kadhaa wa benki hiyo ambao walionekana kuvutiwa na jinsi mashine zinavyotumika kuweka fedha moja kwa moja.

“Hizi mashine za ATM zimekuja wakati mwafaka kabisa hasa kwa wateja wetu ambao wanaendelea na biashara zao wakati matawi mengi yamefungwa, lakini huduma hii itawawezesha kufanya shughuli zao za kibenki za kuweka fedha bila matatizo," aliongeza Neema Munisi, Mhasibu wa tawi la Mlimani City.

Aliongeza: “Tumeanzisha na kuzindua huduma hii ya kuweka fedha kwenye mashine za ATM kwenye matawi manne tu jijini Dar es Salaam na tutaendelea kufungua na kusambaza huduma hii ya kuweka fedha kwenye mashine hizi nchini nzima.”

Kwa upande wake, mteja wa benki hiyo aliyejaribu huduma hiyo mpya, Franscis Momanyi, alisema kwamba kwa huduma hiyo mpya kutoka benki hiyo itawahikishia wateja wote uhakika wa kupata fedha au kuweka fedha wakati wowote pindi watakapohitaji.

Alisema ni muhimu kwa benki hiyo kupeleka kwa haraka huduma hiyo ya kipekee kwenye matawi mengine nje ya Mkoa wa Dar es Salaam ili wateja wengine wapate fursa ya kutumia huduma hiyo

0 comments: