Mama Maria akikabidhiwa tunzo ya amani
“Hivi karibuni tumeshuhudia mambo yaliyotokea bungeni, wananchi
wameona, nilitegemea waliotajwa wangejiondoa wenyewe katika nafasi zao
badala ya kusubiria Rais,” alisema.
Mama Maria alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, mara baada
ya kukabidhiwa tunzo ya amani iliyotolewa na Kamati ya mkesha mkubwa
kitaifa na dua maalum inayotarajia kufanyika nchini Desemba 31, mwaka
huu.
Kauli hiyo ya Mama Maria, inafuatia mjadala mkubwa ulioibuka
bungeni hivi karibuni mjini Dodoma baada ya Wabunge kumtaka Waziri wa
Nishati na Madini. Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo,
Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyuma na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema,
kutakiwa kujiuzulu baada ya kutuhumiwa kuhusika na sakata hilo.
Katika sakata hilo, imedaiwa kuibwa kiasi cha Sh. bilioni 306
zilizochotwa kwenye akaunti hiyo na kuhusisha watu mbalimbali wakiwamo
wafanyabishara na baadhi ya viongozi wa serikali.
Aidha, Mama Maria alisema nchi inahitaji maombi ya pamoja ili
kunusuru taifa kuingia katika machafuko, kutokana na yanayojitokeza hivi
sasa.
Mara baada ya kukabidhiwa tunzo hiyo alisema viongozi wa mwanzo walipewa unyenyekevu na kuweza kupita katika mawimbi na dhoruba.
“Makosa mengine yametokana na uzembe na utu hivyo tunahitaji maombi
ya pamoja mimi naiombea sana nchi yangu, hali tuliyonayo amani kidogo
Mungu anatukumbusha tumkumbuke, tuwe watu wa sala na kazi,” alisema.
Kuhusu vitendo vya ukatili vya kuwaua na kuwajeruhi watu wenye
ulemavu wa ngozi, alisema ni vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo
vinapaswa kukomeshwa.
Aliwataka Watanzania kuhakikisha maombi yao wanayaelekeza kwenye
nchi nyingine ili kuwakomboa na matatizo yanayowakabili ya magonjwa na
vita.
“Tulio wengi katika nchi hii ni watu wenye upendo ni kama
tumependelewa, ndiyo maana nasema viongozi wetu wa awali walipewa
unyenyekevu,” alisema. Alitolea mfano wa baadhi ya mambo yaliyotokea
awali kuwa ni vita vya Kagera ambayo alisema haikuwa kitu kidogo lakini
viongozi waliongozwa kupita kwenye hilo na kuyamaliza. Alisema kwa sasa
yapo magonjwa kama ebola, mabadiliko ya tabia nchi na mambo mengine
ambayo yanahitaji maombi.
Mjumbe wa kamati iliyomkabidhi tunzo hiyo, Askofu wa Kanisa la
Kiinjili la Pentekoste, William Mwamalanga, alisema tunzo waliyompa ni
ya kuhamasisha amani Tanzania.
Alisema tunzo kama hizo wametoa kwa watu mbalimbali na kuwataja
baadhi kuwa ni Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi.
0 comments:
Post a Comment