Saturday, 13 December 2014

Leave a Comment

Idris: Sijajua cha kufanya na milioni 522/- za BBA

 
Mshindi wa Big Brother Afrika, Idrisa Sultan akizungumza katika mkutano na waandishi jana ili kutoa shukrani kwa mashabiki wake. Picha: Halima Kambi
Mshindi wa Big Brother Afrika (BBA) mwaka huu, Idris Sultan amekiri kuwa karibu na baadhi ya washiriki wa kike huku akisisitiza kuwa aliishia katika kuwabusu na si kufanya ngono ndani ya jumba la shindano hilo huku pia akieleza kwa sasa hajui cha kufanya na mamilioni aliyoshinda katika mjengo huo.

Kwa nyakati tofauti kamera zilimnasa Idris aliyeshinda dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 522) akiwa amekumbatiana na baadhi ya washiriki wa kike huku wakionesha kuingia katika ulimwengu wa mahaba.

Katika mahoajino na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Idris alikiri kufanya 'mambo ya chumbani' ndani ya jumba hilo lakini akasisitiza kuwa: "Niliishia kula denda tu, sikufanya kitu kingine zaidi ya hapo."

Alisema wakati mwingine alilazimika kufanya vitendo hivyo kutokana na aina ya watu aliokutana nao pamoja na hali halisi ya maisha ya siku 63 alizokaa ndani ya jumba hilo.

"BBA ni kuonesha namna Waafrika wanavyoweza kuishi kwa pamoja. Kama wewe unaishi kihuni, BBA itakuwa ya kihuni kutokana na aina ya watu wanaoishi mle ndani ya jumba," Idris alisema huku akidai kuwa hana mchumba kwa sasa.

"Ukiwa ndani ya jumba, huwezi kujua Waafrika wanakuchukuliaje. Unalazimika kubadili mawazo kulingana na mtu unayekutana naye ukizingatia kila mtu anakuwa na dhamira yake.

"Wakati ninaondoka nchini kwenda Afrika Kusini kushiriki, watu waliniambia mengi. Wapo walioniambia nikakae karibu na Wanigeria lakini kila kitu ndani ya mjengo ni wewe na tabia zako. Watanzania ni watu wazuri, ukiwa ndani usiishi maisha ya act (kuigiza). Ukiwaona wasichana wanaoga unawaangalia.

"Maisha ya BBA inafikia kipindi yanachosha, kuna kipindi niliwaambia mkiona ninafaa kutoka poa, lakini baadaye nikawa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri," alisema Idris.


MATUMIZI MIL 522/-
Aidha, Idris alisema bado hajajua atazitumiaje Sh. milioni 522 alizopata kwa kuwa mshindi wa BBA huku Ofisa Uhusiano wa Multichoice Afrika, Barbara Kambogi, aliyekuwa amefuatana naye akieleza kuwa wameingia mkataba na Idris wa miezi sita na watampa sapoti katika kila mradi atakaoamua kuufanya.

Idris alisema amepanga kufanya uigizaji wa kuchekesha na kufanya ziara nyingi nje ya mipaka ya Tanzania. 

UHUSIANO WAKE NA LULU
Kuhusu kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii Elizabeth Michael 'Lulu', Idris alisema: "Lulu ni mtu wangu wa karibu, sidhani kama ana mawazo ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi. Ni rafiki yangu tu."

Lulu alijikuta akihusishwa na kuwa na uhusiano wa kimahaba na Idris baada ya kuweka maneno kwenye mitandao ya kijamii yaliyoonekana kama muigizaji huyo wa filamu ya 'The Foolishi Age' amedhamiria kumteka kimahaba mshindi huyo wa BBA.

APUUZA KAULI YA DAVIDO
Idris pia alilitolea ufafanuzi suala lililomponza msanii mkali wa muziki kutoka Nigeria, Davido aliyeponda ushindi wake. Mara tu baada ya Idris kutangazwa mshindi, Davido aliweka maneno kwenye mitandao ya kijamii akidai ushindi wa Idris una udanganyifu.

Hata hivyo, Idris alisema: "Marais wetu wamefanya kazi kubwa kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Nigeria. Nchi hizi zina uhusiano mzuri lakini sisi, vijana tunataka tuuharibu. Ninawasihi suala hili la Davido liishe."

"Davido anafanya kazi nzuri, tunazikubali hadi hapa Tanzania. Tusiendekeze visa visivyokuwa na msingi. Tunapaswa kuonesha upendo kwa kila mtu. Ninachofahamu Davido hakumaanisha vibaya, ilikuwa ni utani ndiyo maana mwishoni baada ya kuona anashambuliwa na watu wengi mtandaoni alisema alikuwa anatania.

"Nilikuwa na Wanigeria mjengoni na wana maneno mengi ya utani, ambayo akiyatamka utadhani anakutukana kumbe anakutania. Ninafikiri tuendelee kutengeneza uhusiano mzuri na nchi nyingine. Tusiwe kama mashabiki wa Manchester United na Arsenal, timu moja ikifungwa, mashabiki wanajinyonga."

AMPA TANO JK
Idris aliyekuwa amefuatana na Mtanzania mwingine aliyeshiriki BBA mwaka huu, Daveda, alimmiminia sifa kemkem Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete 'JK' kwa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya michezo, sanaa na burudani nchini.

"JK amewapa kipaumbele vijana, kama tulivyoshiriki pamoja na Waafrika wengine kumpa ushindi Idris, tusimwangushe rais wetu kwa kuhakikisha tunampigia kura (Happiness) Watimanywa katika shindano la Miss World.

"Dunia sasa imeona kwamba Tanzania tupo, kina Diamond, Jaydee na Prof Jay wanatuwakilisha vyema nje ya nchini. Tunapaswa kuonesha kwamba tupo na tuonekane tunaweza kufanya kitu katika ulimwengu huu," alisema Idris huku akiweka wazi kuwa ni shabiki wa Manchester United ya Ligi Kuu ya England (EPL).

Mtoto huyo wa kwanza kuzaliwa katika familia ya mfanyabiashara Rashid Sultan (Mzigua) na mama Naima Ngido (Mpare), alisema ametulia na kamwe hatakuwa tayari kulitumia fungu lake kupoteza muda na wanawake.

Idris anayechukukia uongo, ana mdogo wake mwenye umri wa miaka 16 aitwaye Khatib na familia yao inaishi jijini Arusha.

Mkali huyo katika kukitema 'Kimombo' (Kiingereza) alisema alianza kufikiri kushiriki BBA akiwa na umri wa miaka 17 lakini mawazo hayo aliishia kuyaweka wazi kwa marafiki zake wa karibu tu.

Kama mshindi wa BBA, Idris alisema amepanga kuitumia fursa hiyo kutetea haki za vijana katika nyanja mbalimbali hasa ya kiuchumi.

"Ukifika Marekani, kijana wa miaka 15 anazalisha na kufanya mambo makubwa lakini hapa kwetu Afrika kijana wa miaka 15 ni kuchezea makopo na kucheza soka na akikosea wazazi wanasema anakua. Lazima tufute dhana hii tukianzia kwa wazazi na vijana wenyewe pamoja na walimu ambao wana muda mwingi zaidi wa kukaa na watoto kuliko hata wazazi," alisema Idris.

0 comments: