Saturday 6 December 2014

Leave a Comment

KIFIMBO CHA MWALIMU NYERERE KILIKUWA NA NGUVU FULANI?

Hayati Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake. KWA miaka mingi watu wamekuwa wakitoa maelezo kadha wa kadhaa kuhusu kifimbo ambacho Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikibeba kila alipokwenda.
Kuna ambao walisema hakikuwa  kifimbo cha kawaida na kuna waliokihusisha kifimbo hicho na zindiko.
Kuna ambao bado wanasema kifimbo cha Nyerere kilikuwa na nguvu fulani ya asili na ya kimila ambayo ilimfanya aheshimike na kuogopwa.
Mwandishi wa vitabu, W.E. Smith, katika kitabu chake kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere, ananukuliwa akizungumzia nguvu za jadi kwenye kabila lake (Nyerere) la Wazanaki.
Katika kitabu hicho Smith ananukuu baadhi ya maoni ya Mwalimu kuhusu nguvu za jadi, hasa katika jamii za Kiafrika.
Anaeleza kuwa Mwalimu, Aprili 1966, aliulizwa kama angeweza kueleza katika lugha ya Kiingereza kuhusu manyoya ya mbuzi ambayo yalichanganywa na nywele zake, ili kusababisha mbuzi aliopewa na ndugu zake aswagwe kwa urahisi hadi nyumbani kwao.
Smith anamnukuu Mwalimu Nyerere akisema: “Nilipokuwa na umri wa kiasi cha miaka 10, siku mmoja baba (Chifu Nyerere Burito) alinituma nifuatane na mke wake wa kwanza, mmoja wa mama zangu wa kambo, kwenda katika kijiji kingine, umbali wa maili nane au kumi hivi, ambako mmoja wa jamaa zake huyo mama, alikuwa amefariki.
“Tulipokaribia kuondoka katika kijiji hicho, kurudi nyumbani, ndugu zake wakampa mbuzi. Lakini mbuzi yule alikataa kutii kuondoka. Na wakati nilipokuwa nakurupushana naye, mmoja wa jamaa za mama yangu wa kambo akasema, ‘usiwe na wasiwasi. Nitakurahisishia kazi.’
“Basi, akang’oa nywele kidogo kutoka kichwani kwangu na manyoya kidogo kutoka katika kichwa cha yule mbuzi. Akazichanganya na mizizi fulani, akatafunia pamoja na halafu akampa mbuzi, akala.
“Akasema ‘sasa mbuzi atakufuata.’ Na kweli mbuzi akanifuata njia yote mpaka nyumbani. Ndiyo, alikuwa ameelekea kabisa. Alinifuata kama mbwa,” anasema Mwalimu katika kitabu cha Smith.
Smith anamnukuu Mwalimu akisema, “Mimi sidhani ni vigumu kama watu wanavyofikiri. Katika maisha ya kikabila, kijana anapofikia umri wa miaka 12 huwa karibu amehitimu. Ndiyo, unajua mambo mengi ya maisha katika umri wa miaka 12 mtu hufundishwa.
“Unayajua yote unayotakiwa uyajue, ambayo hujulikana hadharani. Lakini lazima unafichwa sana siri za wazee.”
Mwandishi anamnukuu Mwalimu enzi hizo akisema kuwa Wakristo wanayakataa mawazo ya kikabila, huku wakiwa na sababu chache za kufanya hivyo, kwa sababu hata wenyewe wanaamini vitu ambavyo haviwezi kuelezeka.
“Ninalofahamu mimi ni kwamba yule mbuzi alinifuata. Na nikijitahidi sana kufikiri naweza tu kusema, sijui,” anaeleza Mwalimu.
Masimulizi kuhusu mbuzi ndiyo yamefanya wengi kuamini kuwa kifimbo cha Mwalimu kinaweza kuwa na nguvu za asili kama nguvu za kufanya mbuzi afuate mtoto kama mbwa, badala ya kuswagwa.
Aidha, ile tabia yake ya kuwa na kifimbo chake popote alipokwenda, iliongeza tetesi na kukuza mjadala. Je, kulikuwa na nguvu yoyote ya kijadi ndani yake?
Bali kuna taarifa kuwa Mwalimu hakuwa na kifimbo kimoja. Makumbusho yake yaliyopo Butiama, Musoma Vijijini, yanaonyesha kuwa vipo vifimbo vyake vingi na mkwaju aliotumia wakati wa kupigania uhuru.
Bado kitendawili hakijateguliwa na bado wanahistoria wana kazi kubwa ya kufanya utafiti wa kifimbo cha Nyerere.

0 comments: