UKOSEFU wa choo kwa muda mrefu ni tatizo linalowakabili watu wengi, lakini kwa bahati mbaya sana miongoni mwa watu wenye tatizo hili hawajui kama lina madhara makubwa na huweza kuwa chanzo cha ugonjwa mkubwa baadaye unaoweza kusababisha hata kifo.
Kwa kawaida, binadamu anatakiwa kwenda haja kubwa kila siku, angalau mara moja kama siyo zaidi ya mara moja, kulingana na aina ya chakula na kazi anazozifanya kwa siku. Anapopitisha siku moja bila kwenda haja kubwa, ili hali amekula kama kawaida, aelewe kwamba kuna dosari tumboni.
Madhara ya ukosefu wa choo kwa muda mrefu ni pamoja na kupatwa na maumivu makali ya tumbo, magonjwa ya moyo, kupatwa na kiharusi na kujikunja kwa utumbo ambako huweza kusababisha kifo kama hali hiyo haitaweza kushughulikiwa mapema na kwa usahihi.
Kujiepusha na madhra yatokanayo na ukosefu wa choo wa muda mrefu ni rahisi sana. Ili kujiepusha na tatizo hilo, unatakiwa kuzingatia kanuni ya kwanza ya KUNYWA MAJI kwa wingi kila siku. Hakikisha kwa siku unakunywa maji ya kutosha, kiasi cha lita moja hadi lita tatu au zaidi, kutegemeana na kazi unazozifanya.
Aidha, kanuni ya pili, ambayo nayo ni rahisi ukilinganisha na madhara utakayoweza kuyapata kwakuacha kuifuata, ni ulaji wa vyakula vyeye kamba lishe ya kutosha (fibre). Utapata kamba lishe ya kutosha kwa kula matunda na mboga za majani kwa wingi. Matunda kama parachichi, machungwa, embe, papai, nafaka zisizokobolewa ni miongoni mwa matunda na vyakula vyenye ‘fibre’ za kutosha.
Usidhani ulaji wa matunda na mboga za majani ni anasa, bali ni jambo la lazima kwa sababu ni uhai wako. Kwa kunywa maji mengi, kutarahisisha usagaji wa chakula tumboni na kufanya upitaji wa sumu na uchafu mwingine kwenye utumbo wakati wa kutoka kama haja kubwa kuwa rahisi na laini.
Kwa muhtasari unaweza kusema chanzo kikubwa cha ukosefu wa choo ni tabia ya kutokupenda kunywa maji mengi na kutokula matunda, mboga za majani pamoja na nafaka zisizo kobolewa mara kwa mara, kama siyo kila siku. Kwa upande mwingine, adui mkuwa wa ukosefu wa choo, ni maji na lishe ya matunda na mboga za majani pamoja na nafaka zisizokobolewa.
Hivyo, utendee haki mwili wako nao ukutendee haki kwa kukulinda dhidi ya maradhi hatari kwa kupenda kunywa maji ya kutosha kila siku, bila kujali kama unasikia kiu ama la, kwani maji ni uhai na ni tiba bora kuliko zote.
0 comments:
Post a Comment