Showing posts with label jamii. Show all posts
Showing posts with label jamii. Show all posts

Sunday, 28 December 2014

MWAKA 2014 UNAISHIA NA HUJAFANYA CHA MAANA, WHY? KWA NINI?

Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa upendo aliouonesha kwangu na kuniwezesha kuiona siku ya leo nikiwa mzima. Nadiriki kushukuru kwa sababu, wapo waliotamani kuiona wiki hii wakiwa wazima lakini baadhi wameshaondoka kwenye ardhi hii huku wengine wakiwa hoi mahospitalini na majumbani. Ndugu zangu, mwaka ndiyo huo unakaribia kuisha. Najua wapo wanaoumaliza wakiwa wamefanya mambo makubwa lakini pia wapo ambao mioyo yao imesinyaa kwa kuwa, waliyopanga kuyafanikisha hayakutimia.
Mimi nataka kuwatia moyo wale ambao mwaka unaisha bila kufikia mafanikio waliyotarajia. Kumbuka kila jambo linapangwa na Mungu, yawezekana yeye kwa sababu anazojua kapanga ufanikiwe mwaka ujao na siyo huu.
Kikubwa ni kuamini kuwa hakuna linaloshindikana kwako. Wewe ni bilionea mtarajiwa! Wewe ni mmiliki wa makampuni makubwa mtarajiwa nk. Hizo ziwe ni kati ya ndoto zako kubwa kwenye maisha yako ya kesho na huna sababu ya kufa moyo.
Ukifuatilia historia za watu wenye mafanikio makubwa duniani utagundua miaka na miaka ilikatika wao wakiishi maisha magumu lakini hawakunyanyua mikono juu na kusema wameshindwa!Kadiri walivyokuwa wakikumbana na changamoto ndivyo walivyozidi kupambana wakiamini walikuwa wakiyakaribia mafanikio.
Kwa jitihada walizoonyesha kuna wakati Mungu akaamua kuwabandika mikono ya baraka na wakafanikiwa. Wewe pia amini mwaka ujao ni wako wa mafanikio, ongeza bidii.
Hata hivyo, yapo mambo ya msingi ya kuyazingatia ili mwaka ujao ujiweke kwenye nafasi nzuri ya kuingia kwenye historia ya watu waliofanikiwa.
Ni vyema ukajipanga upya
Waswahili wanasema, kuteleza si kuanguka, kama ulishindwa kufanikiwa mwaka huu, kaa chini tena na uorodheshe malengo yako. Unashauriwa kutafakari upya na kutafuta njia sahihi za kuweza kufanikisha malengo hayo.
Thubutu tena na tena
Maisha siku zote ni mapambano. Maisha ni kutoogopa kujaribu kwa kuhofia kushindwa.  Kamwe usiogope kuthubutu tena na tena kwani hata ukishindwa itakuwa ni hatua ya kuelekea kwenye mafanikio.
Dadisi, ongea na waliofanikiwa
Kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine ambao wamemaliza mwaka huu wakiwa wamefanikiwa katika mambo yao. Jaribu kudadisi na kung’amua ni kwa namna gani wameweza kufikia malengo yao ili na wewe ujifunze kitu kutoka kwao.
Kukata tamaa ni mwiko
Katika kujaribu kufikia malengo yako ni wazi umekutana na vikwazo vya hapa na pale na wakati mwingine kuhisi huwezi kuendelea tena.
Siku zote vikwazo unavyokutana navyo viwe ni changamoto kwako ya kujipanga upya na kuanzisha tena mapambano ya kufikia malengo yako.
Kukata tamaa ni mwiko kwani inaelezwa kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi maisha yasiyokuwa na nyuma wala mbele wameathiriwa na tabia ya kukata tamaa.
Omba ushauri
Katika mbio za kufikia malengo yako, usiishi kama kisiwa, wakati mwingine omba ushauri wa kimawazo pale utakapokwama.  Usikubali kubaki na msongo wa mawazo, jaribu kutafuta msaada na ushauri kwa watu unaowaamini.
Anasa ni sumu
Matumizi mabaya ya fedha na kupoteza muda mwingi katika mambo ya anasa kamwe haviwezi kukusaidia kutimiza ndoto zako.  Daima kazi kwanza, starehe baadaye, ishi kama mtumwa leo, ili utimize ndoto ya kuishi kama mfalme kesho!
Jifanyie tathimini
Katika hatua nyingine ni vyema pia ukachukua muda wako kujitathimini kwa kudadisi sababu ambazo huenda zimekufanya usifanikiwe mwaka huu. Je, matumizi yako ya fedha yalikuwa mabaya kiasi cha kutokuwa makini na kila shilingi uliyokuwa ukiipata? Je, hukujituma sana na hukutumia akili na maarifa yako katika kiwango cha juu?
Je, ulitengeneza mazingira ya kuwapa mwanya maadui wakukatishe tamaa na kukufanya uhisi huwezi? Fanyia kazi maswali hayo!
+

Wednesday, 17 December 2014

UNATAKA KUPATA UTAJIRI WA HARAKA? SOMA HAPA

HAISHANGAZI kama ukilala maskini ukaamka tajiri. Swali ni je, utaufanyia nini utajiri huo? Amini usiamini inawezekana. Kumbuka, sijasema itakuwa rahisi, nilichokisema ni kwamba inawezekana. Hapa nakuletea dondoo za namna ya kupata utajiri haraka kwa lugha ya mtaani fastafasta.
WEKEZA
Anza kuwekeza ukiwa mdogo yaani kiumri na kidogo ulichonacho. Inawezekana ukaanza hata ukiwa shule ya msingi au hata kama ni shule ya awali sawa tu. Kinachohitajika ni mazingira rafiki ya ujasiriamali. Nakuhakikishia kuwa fedha zako zitaongezeka kila kukicha ukizingatia mambo mengine nitakayoeleza baadaye.
Ni kama mayai yanayotagwa na ndege ambayo baadaye huatamiwa na kuzalisha ndege wengine.
Angalizo; kama unafuatilia makala haya wakati umri umekutupa mkono na hukuweza kuanzia shule za awali lakini una watoto, unaweza kuwatumia kwa kuwatengenezea mazingira ninayoyaeleza. Uwe mwalimu wa ujasiriamali kwa watoto wako au hata wajukuu zako.
Hata kama umri umekwenda lakini Mungu kakujalia kibarua, jaribu kuwekeza asilimia 50% ya mshahara wako katika kujitoa kwa kiwango cha hali ya juu kabisa kutokana na mfumuko wa bei katika soko huru na ugumu wa maisha.
Una uwezekano wa asilimia 50 kwa 50 kutengeneza utajiri au kuanguka ndani ya siku 90.

OA AU OLEWA NA MTU TAJIRI
Najua hapa utakuwa na maswali mengi kwamba nisipooa au kuolewa na mtu tajiri basi nitakufa masikini. Inawezekana pia japo ni kwa asilimia ndogo! Twende mbele zaidi, yaani usemi huu unamaanisha uwe na mwenza wa maisha mwenye maono. Yawezekana msiwe na utajiri kwa maana ya fedha lakini mkawa matajiri wa mawazo ya kijasiriamali. Pale mmoja anapofikia ukomo wa mawazo na kuhisi kushindwa, basi mwenza wake awe nguzo ya kushauri na siyo kukatisha tamaa kabisa kuwa sasa tumeshindwa! Hapana, muote ndoto tofauti lakini mshirikiane kuzitafsiri ili kufikia mafanikio.

SHINDA BINGO
Hii haimaanisha kuwa utajiri unatokana na michezo ya kubahatisha pekee lakini pia inawezekana ila ni kwa asilimia ndogo. Kumbuka wapo waliozaliwa na bahati zao wakashinda michezo ya kubahatisha wakawa matajiri, mifano ipo. Falsafa ni kwamba ujijengee tabia ya kujaribu kufanya vitu. Hapa narudi kipengele cha kwanza yaani kuwekeza hata katika kitu ambacho huna hakika kama utafanikiwa.
Wajasiriamali wanasema ‘ku-take risk’. Haitashangaza kuona unafanikiwa ghafla na wasiamini katika kujaribu wakaishia kusema unatumia ndumba.
WAZAZI MATAJIRI
Kama umezaliwa katika familia tajiri, ukawa na maono katika ujasiriamali, wewe upo nusu ya safari ya mafanikio. Unachotakiwa kufanya ni kuwa mtiifu kwa kupita kwenye nyayo za baba na mama ukiwashawishi kwa kuwa mwangalifu katika matumizi ya kile wanachokupatia. Usitumie kwa kutupatupa ili wakitangulia mbele ya haki ubaki kuwa vizuri tofauti na inavyotokea kwa baadhi ya familia. Jenga nao ushirikiano wa hali ya juu na wakati mwingine wape mawazo hata kama watayaona ni ya kitoto lakini utakuwa umejijengea mazingira ya wao kukuona sehemu ya utajiri wao.

NENDA SHULE UPATE UJUZI
Elimu ni mtaji mkubwa kuliko hata fedha. Jitahidi kusoma katika mazingira yoyote bila kujali wingi wa miaka utakayopoteza darasani. Jaribu kupata weledi na ujuzi wa kila namna halafu chagua kimoja ambacho kitakupa fedha nyingi.
Itaendelea wiki ijayo.
+

Bonge la ‘byutful’ kutoka Ethiopia!


HUYO ni mrembo kutoka watu wa jamii ya Surma nchini Ethiopia ambayo inajumuisha makabila ya Suri, Mursi na Me’en.  Bila shaka anavutia japokuwa anashitua kidogo!  Jamii ya watu hao iko Kusini mwa nchi hiyo na ni wafugaji kama walivyo Wamasai nchini Tanzania.

Kwa kifupi, ili kupata urembo huo, mdomo wa chini wa mwanamke hutobolewa na kuwekwa kijiti kidogo, na unapopona huwekwa kijiti kikubwa zaidi na zaidi hadi kisahani kikubwa cha mbao kama kinavyoonekana.

Hivyo mdomo huzidi kupanuka zaidi na kuvutia zaidi.  Huenda hufikia kiasi cha kutisha au kuogopesha – hii ni kwa mtazamaji asiyekuwa wa jamii ya Surma.  Hili huenda sambamba na kung’olewa kwa meno mawili ya chini ili kuruhusu uwekaji wa visahani hivyo vya miti au udongo.

Urembo huo huanzishwa kwa msichana akifikia miaka 14 au 15 ambapo hufichwa mahali maalum na kufanyiwa hivyo.  Mwenye mdomo mkubwa zaidi ndiye hupata mahari kubwa zaidi ya ng’ombe! Hivyo, wazazi hujitahidi kuipanua midomo ya mabinti zao kiasi iwezekanavyo.

Hata hivyo, historia inasema kwamba, ili kukwepa wanawake wao kuchukuliwa na wafanya biashara ya utumwa kutoka nje, midomo yao “ilivurugwa” hivyo ili wakamata watumwa wasiwe na hamu ya kuwachukua na kuwapeleka utumwani.

Ni utamaduni unaofurahisha, au siyo?  Kwa vile tunaishi katika utandawazi, si vibaya kuujaribu utamaduni huo.
+

Monday, 15 December 2014

ACHA KULA UJANA, PAMBANA SASA KUSAKA MAFANIKIO!

Niwakumbushe tu kwamba, licha ya sarakasi zote tunazofanya kwenye maisha yetu ya kila siku, ni vyema tukamtanguliza Mungu na kufanya yale ambayo ametuamrisha na kuachana na aliyotukataza. Kwa kufanya hivyo atatubariki na mambo yetu yatatunyookea.
Baada ya kusema hayo, sasa nirudi kwenye mada yangu ya wiki hii. Mpenzi msomaji wangu, ukweli ni kwamba kila mmoja wetu angependa kuwa na maisha mazuri au kifupi kwamba awe na fedha nyingi, kwa maana ya tajiri.
Hii ndiyo sababu mara kadhaa umepata kusikia juu ya watu wanaosaka utajiri kwa njia mbalimbali, zikiwemo haramu na ushirikina.
Katika dhana ya kusaka mafanikio, kama lengo la kila mmoja ni kutafuta kazi za ndoto zake au kuanzisha kampuni mpya, vijana wengi wanaweza kuweka malengo yao na kufanikiwa haraka kama wataamua.
Wapo watu wengi waliofanikiwa kushika kiasi cha shilingi milioni moja ya kwanza maishani mwao wakiwa na umri chini ya miaka 30 na hapo ndipo mawazo ya wao kuwa mamilionea yalipochipukia. Hakuna uchawi wowote waliowahi kuufanya ili kuwafikisha walipo sasa.
Nafahamu kwamba inawezekana kuwa na maisha mazuri mapema katika maisha yako kama kweli umedhamiria na ukaamua kupigana.
Kama mfanyakazi kijana, watu wengi watauona umri wako kama tatizo kubwa la kufikia malengo yako. Lakini ukweli ni kwamba ujana wako unaweza kuwa na msaada mkubwa sana kwako.
Wengi niliowahi kufanya nao kazi na biashara walikuwa ni watu wazima, wakati mwingine walikuwa wakubwa kuliko mimi.
Hawa wote walikuwa wanataka kufikia malengo yao lakini baadhi hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kufika huko wanakofikiri.
Walihitaji kutokea kwa mtu mwenye dhamira na nia anayeifahamu vyema biashara wanayotaka kuifanya.
Hata hivyo, bado kuna hasara pia kwa kuwa kijana na mtu asiye na uzoefu katika kazi au ujasiriamali, lakini unapoamua kukubali umri wako na kuazimia kupigana kuelekea mafanikio, lazima uwaambie watu unaotaka kushirikiana nao kuwa wewe kweli ni kijana, lakini hilo halimaanishi kwamba huelewi unachokifanya, unajua na umedhamiria kuwa bora katika uwanja unaoingia.
Unapobaini kipaji chako, ni lazima ujitoe kukitumia ili kiweze kukupa maisha unayotamani. Na katika hili, usiwe mtu wa kuwa peke yako kimawazo, jaribu kushirikiana na unaowaamini katika mawazo yako, kwamba unafikiri kuhusu kufanya hivi na vile, wasikilize wanavyokushauri, lakini mwisho wa siku ni lazima uamue kwa faida yako mwenyewe.
Nina uhakika yupo mtu sahihi, bila kujali umri wake ambaye mara nyingi hutokea kuwa mkubwa kuliko wewe, atakayekubaliana na mawazo yako na kuamua kuungana na wewe katika kuyafanyia kazi.
Niseme tu kwamba, wewe kijana huu ndiyo muda wako wa kupambana na kusaka mafanikio kwa nguvu zote.
Waliocheza enzi za ujana wao, sasa wanakiona cha mtemakuni. Acha kula ujana, tengeneza maisha yako ya baadaye sasa!
+

Saturday, 13 December 2014

SHITUKA WEWE! UTAISHI KWENYE NYUMBA YA KUPANGA MPAKA LINI?

Maisha siku zote ni kuwa na malengo, namaanisha malengo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Kwamba unaishi huku ukijua mwaka huu utafanya jambo flani na mwaka kesho utafanya jambo flani.
Cha ajabu sasa wapo watu ambao hawana malengo yoyote, wanaishi ili mradi siku zinakwenda.
Hili ni tatizo na ukijaribu kufuatilia utagundua wote wanaoishi bila malengo wana maisha magumu na wameridhika nayo. Yaani hawajui kesho yao itakuwaje na wala hawataki kujishughulisha kujua.
Ilimradi leo Mungu kawajaalia wamekula, wanaona hawana sababu ya kufikiria kesho watakula nini. Hii ni shida!
Katika hilo leo nataka kuwazungumzia wale wenzangu na mimi ambao tunaishi kwenye nyumba za kupanga. Ukifuatilia sana utagundua ni wachache sana ambao hawakuwahi kuishi kwenye nyumba za kupanga, hasa maeneo ya mjini.
Naweza kusema hiyo ni hatua ya tulio wengi katika kuelekea kwenye kumiliki nyumba zetu. Hapa namaanisha kwamba, wengi wetu tumeanza maisha tukiwa tumepanga chumba kimoja, baadaye tukachukua chumba na sebule na hatimaye tukapanga nyumba nzima kadiri vipato vyetu vilivyokuwa vinaongezeka na familia kuwa kubwa.
Lakini katika maisha ya sasa utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakuwa unawaza kupanga tu na wala hufikirii siku moja kuwa na nyumba yako na ikiwezekana uwapangishie wengine.  Nasema haya nikimaanisha kwamba, wapo watu huko mtaani ambao wao wamechukulia maisha ya kupanga kama sehemu ya maisha yao. Yaani hawawazi kumiliki nyumba, walipokuwa mabachela, walipanga, walipooa bado waliendelea kupanga na huenda sasa wana familia lakini bado wanapanga na hawana mikakati ya kuwa na ‘mijengo’ yao.
Walio katika mazingira hayo wajue wanajiandaa kuzeeka wakiwa kwenye nyumba za kupanga, jambo ambalo ni baya sana. Ifike wakati ukae na kujiuliza kwamba, wale ambao walianza kwenye nyumba za kupanga lakini sasa wanaishi kwenye nyumba zao huku nao wakiwa na wapangaji wao wana kipato gani kikubwa kukushinda wewe?
Marafiki na wafanyakazi wenzako ambao huenda mnapokea mshahara sawa wamejenga, wewe pesa zako zinaishia wapi? Au unaona kujenga siyo ishu? Kwamba hata usipojenga ilimradi una sehemu ya kuishi na mambo yanakwenda sawa, basi poa?
Mimi nadhani unakosea, kumbuka ipo siku utakuwa huna pesa ya kupanga, nguvu zimeisha na una familia ambayo inahitaji uihifadhi. Kama utakuwa hujajijengea kakibanda kako katika wakati huu ambao una kazi na Mungu anakujaalia unapata vijisenti, huoni ipo siku utajuta?
Mimi nakushauri kwamba, kama unafanya kazi au una vipato vingine na hujajenga, wala huna malengo hayo, ni vyema ukaanza sasa. Weka mikakati ya kuhakikisha unakuwa na nyumba yako. Jinyime kama wanavyofanya wenzako. Kumbuka ni wachache sana ambao walijenga baada ya kupata pesa nyingi, wengi walidhamiria siku moja kuachana na mambo ya kupanga, wakawekeza kidogokidogo, mara wakanunua viwanja, wakaanza msingi na hatimaye kusimamisha nyumba. Sasa wanaishi kwao na wengine ni baba wenye nyumba/mama wenye nyumba, kinachokushinda wewe ni kipi?
Tena mbaya zaidi baadhi ya waliojenga nyumba zao unaweza kukuta wanapata pesa ndogo kuliko hizo unazopata wewe, huoni umefika wakati wa wewe kufikiria kuwa na nyumba yako? Tafakari kisha ni vyema ukachukua hatua.
+

Saturday, 6 December 2014

RAHA YA MAFANIKIO YAKO USAIDIE NA WENGINE WAFANIKIWE!

Mpenzi msomaji wangu, unapojaaliwa kuwa na mafanikio jambo la kwanza unatakiwa kumshukuru sana Mungu pamoja na wale ambao kwa namna moja ama nyingine wamekufanya ufike hapo ulipo.Huwezi kufanikiwa kwa ujanja wako, mafanikio yako yote nyuma yake kuna mkono wa Mungu. Yeye ndiye anayeweza kuziona jitihada ulizonazo na akaona akutimizie ndoto zako. Ukiacha yeye, wapo watu mmojammoja au kwa vikundi na taasisi ambao wamechangia wewe kuwa na mafanikio uliyo nayo. Hawa ni watu wa kuwaheshimu sana. Kamwe usiwasahau, endelea kuwa nao karibu kwani umuhimu wao kwako ni mkubwa sana.
Aidha, unapofanikiwa na wewe unatakiwa kuwa chachu ya mafanikio kwa wengine. Unatakiwa kuwashika mkono ndugu, marafiki na watu wengine wanaokuzunguka ili watoke kwenye hali duni walizonazo. Ukifanya hivyo utazidi kupaa kimafanikio na hata siku moja huwezi kuporomoka.
Ipo mifano mengi ya watu ambao wamefanikiwa lakini wanakosa furaha kuwaona watu wanaowazunguka bado wanaogelea kwenye dimbwi la umasikini.Hawa utawaona wakiwa mstari wa mbele kuwasaidia wengine kimawazo na hata kifedha ili nao wainuke na waweze kutimza ndoto zao.
Iko wazi kwamba bosi wangu, Eric Shigongo ni miongoni mwa watu wenye mafanikio makubwa. Kama uliwahi kusoma popote kuhusu historia ya maisha yake, utaona ni jinsi gani amepambana kufika hapo alipo.
Kinachotia moyo zaidi ni kwamba, licha ya mafanikio aliyonayo, hajaridhika, bado anaendelea kupambana na kuzidi kujiwekea malengo makubwa zaidi.
Lakini licha ya mafanikio yake, bosi wangu huyu ambaye pia ni mwalimu wa ujasirimali amekuwa akitumia muda wake mwingi kutoa elimu kwa watu mbalimbali juu ya namna wanavyoweza kutoka kwenye umaskini na kuingia kwenye utajiri.
Amekuwa akifanya hivyo kupitia vitabu vyake, kwenye makongamano na semina mbalimbali akieleza njia ambazo yeye amepita mpaka akafikia hapo alipo sasa. Ukiacha elimu anayotoa, pia amekuwa akiwasaidia wengi kifedha ili waweze kutimiza ndoto zao. Hiki ndicho ambacho watu waliofanikiwa wanatakiwa kukifanya.
Huwezi kuendelea kuwa kwenye mafanikio kama utakuwa mchoyo wa kuwafanya na wengine wafanikiwe. Utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakuwa unataka ufanikiwe wewe tu na wengine waendelee kuwa mafukara.
Hivi utakuwa ni mtu wa aina gani kama una pesa nyingi lakini umekuwa mgumu kuwasaidia wale ambao wanahitaji msaada kutoka kwako? Faida ya wewe kufanikiwa ni ipi sasa kwa jamii yako?Mimi nadhani kuna kila sababu ya wale ambao wamefanikiwa kuona wana jukumu la kuwasaidia na wengine kufanikiwa.
Kama si kwa kuwapa mitaji basi hata kwa kuwapa mawazo ambayo yanaweza kubadili fikira zao.
 Usijenge mazingira ya kwamba wewe tu ndiye unayestahili kuishi vizuri, wasaidie na wengine waishi maisha ya furaha. Kumbuka faida ya kufanya hivyo ni kubwa sana.
Kwanza Mungu atakuongezea mafanikio yako na utashangaa kila unalolipanga linatimia. Pia, jamii inayokuzunguka itakupenda na itakuona ni mtu unayejali wengine.
Kwa maana hiyo unapofanikiwa usijitenge na jamii inayokuzunguka. Saidia pale inapopidi, washike mkono wengine waweze kusimama. Kumbuka siku wakiwa wamefanikiwa, ile tu kusema ‘flani kanisaidia mimi kufika hapa’, Mungu anakuzidishia baraka na unashangaa mambo yanazidi kukunyookea.
+