Mshindi wa Big Brother Hotshots, Idris akionesha
mfano wa hundi ya Dola 300,000 aliyokabidhiwa juzi baada ya kuibuka
kidedea katika shindano hilo lililodumu kwa siku 63 nchini Afrika
Kusini.
Idris aliyeingia fainali pamoja na washiriki wengine nane baada ya kudumu katika mjengo huo kwa siku 63, alitangazwa mshindi baada kupigiwa kura nyingi kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika na watazamaji waliokuwa wakifuatilia kwa kina shindano hilo.
Kwa ushindi huo, Idris amejinyakulia kitita cha Dola za Marekani 300, 000 sawa na Sh. milioni 522 za Tanzania (kiasi hicho ni kulingana na viwango vya dola ya Marekani sokoni jana kwa thamani ya shilingi ya Tanzania), hivyo Mtanzania wa pili kushinda shindano hilo baada ya Richard Bezuindenhout aliyeshinda 2007.
Akizungumza na NIPASHE jana, Meneja Uhusiano DStv Tanzania, Barbara Kambogi alisema wamefurahishwa na ushindi wa Idris kwa kuwa ameiwakilisha vema Tanzania na kuwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpokea keshokutwa, Jumatano.
"Kesho (leo) nitatoa ratiba kamili ya kuwasili kwake, ila atakuja Jumatano, kwa sasa naendelea kufuatilia ili kujua ratiba kamili," alisema Barbara ambaye kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa DStv Tanzania waliendesha kwa makini mchakato wa kumpata Idris aliyeipeperusha vema bendera ya Tanzania.
Idris ambaye anakuwa mshindi wa msimu wa tisa tangu kuanzishwa kwa shindano hilo, alikutana na ushindani mkali kutoka kwa washiriki wengine 25 katika wiki tisa alizokaa mjengoni humo kabla ya baadaye kubaki nane walioingia fainali.
Baada ya kutangazwa mshindi Idris alisema anajisikia kuchoka baada ya “safari ndefu”. “Nampenda kila mmoja Afrika, nitaendelea kujitoa kwa ajili yao kila siku,” alisema kijana aliyeiwakilisha vema Tanzania akitokea mkoani Arusha.
Washiriki nane walioingia fainali kabla ya Idris kuibuka bingwa ni Butterphly, M’am Bea, JJ, Sipe, Nhlanhla, Macky2 na Tayo kutoka Nigeria ambaye naye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda.
Mkurugenzi wa M-Net Kanda ya Afrika Magharibi, Wangi Mba-Uzoukwu, alipongeza kwa namna mchakato mzima wa shindano hilo ulivyoendeshwa hadi kupatikana kwa mshindi, Idris.
”Nampongeza Idris kwa kuwa mshindi wa Big Brother Hotshots – na ninawashukuru washiriki wengine wote kwa kuweza kutoa burudani kwa bara letu kwa siku 63.”
0 comments:
Post a Comment